Haaland azua hofu kisa Arsenal

Muktasari:

  • Haaland alikosa mechi tisa mwanzoni msimu huu baada ya kuumia mguu. Alirejea uwanjani mwishoni wa Januari na tangu wakati huyo amecheza mechi nane za Ligi Kuu England na kufunga mabao manne.

Manchester, England. Straika, Erling Haaland amewapa hofu mashabiki wa Manchester City baada ya kushindwa kuendelea na mazoezi alipokuwa na kikosi cha timu ya taifa ya Norway.

Straika huyo wa Man City, mwenye umri wa miaka 23, alijiunga na timu yake ya taifa kwa ajili ya mechi za kirafiki dhidi ya Jamhuri ya Czech na Slovakia.

Fowadi huyo alionekana kuumia mazoezini. Picha zilionyesha, straika huyo mwenye kimo cha futi 6 na inchi 4 akitoka kwenye uwanja wa mazoezi huku akishikilia mguu wake.

Man City itakuwa nyumbani Etihad kucheza na Arsenal katika mchezo muhimu kabisa wa kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England baada ya mapumziko ya kupisha Kalenda ya Fifa.

Man City chini ya Pep Guardiola itaingia uwanjani kwenye mechi hiyo ikiwa imezidiwa pointi moja na Arsenal. Hata hivyo, kilichoelezwa na daktari wa Norway kinawaondoa hofu mashabiki wa Man City na kuamua mkali wao huyo atakuwapo hiyo siku ya kuwakabili Arsenal.

Haaland alikosa mechi tisa mwanzoni msimu huu baada ya kuumia mguu. Alirejea uwanjani mwishoni wa Januari na tangu wakati huyo amecheza mechi nane za Ligi Kuu England na kufunga mabao manne.