Dk Killimbe arudishwa TCRA mwaka mmoja baada ya kutenguliwa

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Jones Killimbe.

Muktasari:

  • Dk Jones Killimbe ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amemrudisha Dk Jones Killimbe katika wadhifa wa Uenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), mwaka mmoja baada ya kumtengua.

 Dk Killimbe alitenguliwa katika wadhifa huo Septemba mwaka jana na nafasi yake alipewa Mhandisi Othman Khatib.

Hatimaye Khatib naye hakudumu katika nafasi hiyo, Novemba 7, mwaka huu Rais Samia aliivunja bodi hiyo iliyokuwa ikiongizwa naye.

Hata hivyo, Dk Killimbe anateuliwa ikiwa ni siku sita tangu Rais Samia aivunje bodi ya TCRA iliyokuwa ikiongozwa na Khatib.

Aliyekuwa Makamu mwenyekiti wa bodi hiyo ni Khalfan Saleh na wajumbe ni Dk Mzee Suleiman Mndewa, Fatuma Simba, Ikuja Abdallah, Batenga Katunzi na Rehema Khalid.

Uteuzi huo umetangazwa leo, Novemba 13, 2023 kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus.

Mbali na Dk Kilimbe, Rais Samia pia amemteuwa Juma Reli kuwa Makamu Mwenyekiti wa bodi hiyo.

Dk Kilimbe ni mtaalamu mawasiliano mwenye shahada ya uzamili katika taaluma hiyo.

Kabla ya awamu hii, Dk Kilimbe aliteuliwa na Hayati John Magufuli Novemba 25, 2016 kuiongoza bodi hiyo.