Namna ya kujilinda kiuchumi tunapoelekea mwisho wa mwaka

Tuna siku chache kabla ya mwisho wa mwaka 2023. Je, hali yako ya kifedha ikoje? Mwaka mpya unakuja, na Januari ina mambo mengi yanayohitaji fedha. Mwisho wa mwaka kuna mambo mengi pia yanayohitaji fedha.

Ni wakati wa likizo za wanafunzi na pia wafanyakazi wengi, na wafanyabiashara wanachukua likizo. Wengine wanaenda kusalimia wazazi wao vijijini, wakiwa na watoto, ndugu na jamaa. Ni wakati wa maandalizi ya safari na kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka.

Wakati wa maandalizi ya mwisho wa mwaka ni vyema kujua mambo ambayo unaweza kuyafanya kuokoa fedha na kutumia vizuri rasilimali fedha uliyonayo au uliyopanga kuifikiria. Kuna mambo matatu yanayoweza kukusaidia.

Mosi, Angalia kama ulitengeneza bajeti na ukapanga utumie kiasi gani kwenye sikukuu na likizo za mwisho wa mwaka. Hata kama hujaandaa bajeti mwanzoni hujachelewa, jaribu kuchanganua gharama zako.

Kwa mfano, unasafiri na nani, kwenda wapi, kwa muda gani, utatumia gharama gani na nyumbani kwako utapaacha katika hali gani, na utasafiri kwa usafiri gani, na gharama zake zikoje.

Hapa utapata gharama, halafu utaangalia wewe una kiasi gani cha fedha. Je, kiasi hicho cha fedha kinatokana na nini? Akiba uliyojiwekea? Kama ni mkopo – ushauri ni kuwa usitumie mkopo kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka au sherehe zozote.

Unaweza kuuza sehemu ya uwekezaji wako kama hisa kupata fedha. Ni vizuri kujiuliza kama ukitumia kiasi cha fedha ulichopanga unaweza pia kuwa na uwezo wa kulipia gharama za mwanzoni mwa mwaka ujao.

Pili, Fikiria unaposafiri, kama utatumia gari binafsi jaribu kuliweka katika hali nzuri, fanyia matengenezo na majaribio kabla ya kuanza safari ndefu. Kama hujawahi kuendesha safari ndefu tafuta dereva mwenye uzoefu. Ukitengeneza gari lako tengeneza kwa fundi wa uhakika wakati huu mafundi ni wengi pia.

Hakikisha gari lako lina bima na lina vifaa vyote vinavyohitajika kwa ajili ya usalama wako, abiria na watumiaji wengine wa barabara. Endesha kwa staha na spidi ya kawaida, hakuna haraka unapoelekea likizo. Kama unasafiri kwa basi ama kwa treni panga mapema, kata tiketi angalau wiki moja au mbili kabla ya safari kuepusha kulanguliwa tiketi ama kukosa nafasi.

Tatu: Angalia hali ya afya ya familia yako. Angalia kama una bima ya afya ambayo ipo hai. Kata bima ya safari. Kama unatumia gari kuna vituo vya mafuta ambapo ukinunua mafuta na kulipia kupitia mifumo ya malipo ya kidijitali hapohapo unapata bima ya safari kwa siku kadhaa.

Kama unatumia usafiri wa mabasi ama treni unaweza kukata bima vocha ya Sh200 tu kwa mtu mmoja na inadumu kwa siku 3 za safari. Bima ni muhimu, kwani kwenye safari kunaweza kuwa na majanga mbalimbali ambayo bima hiyo inaweza kukukinga wewe na familia yako. Kujua namna ya kupata bima hizi ni vizuri kuwasiliana na makampuni ya bima ama benki yako.